Thursday, April 9, 2009

ya kale ni dhahabu kweli?

Mzee Ndejembi

Wazee vingine hatukubaliani
Nadhani wengi miongoni mwetu, nina maana, wale ambao ni vijana, tulipokuwa tunakua tulifundishwa kuwaheshimu na kuwatii wazee wetu. Mara nyingi neno lao lilikuwa ni amri, yaani, kama sheria.
Kwa sisi vijana, hata kama pale ambapo tulikuwa hatukubaliani nao kabisa, tullikaa kimya tu. Na kutokana na hekima zao wazee wetu nyakati hizo, waliweza kujua kama wamekubaliwa ama wamekataliwa.
Juzi wazee wanne waliokuwa katika CCM zamani, wakiongozwa na Mzee Pancras Ndejembi, waliita waandishi na kutuambia jinsi wanavyoona wao kuwa nchi iendeshwe.
Wazee hawataki Rais Kikwete apingwe katika uchaguzi wa mwaka 2010. Sawa kabisa! “Utaratibu wetu ndani ya chama unafahamika; Mwinyi tulimpa miaka kumi, Mkapa naye vile vile, lipi baya alilofanya Kikwete hata tumnyime asiendelee kwa kipindi kingine?” alihoji Mzee Ndejembi.
Ni haki yao. Lakini wakati wazee, ambao tunategemea wamejaliwa na hekima, wakisema hivyo nao wajue kuwa na sisi wananchi wengine wa Tanzania, tuna haki yetu vile vile.
Sijui wazee wamesahau kuwa kuna Katiba? Kwa hoja ile ile ya kuheshimu Katiba yetu inayotamka wazi kabisa kuhusu haki ya kupiga kura au kupigiwa kura kwa kila raia wa Tanzania, ukiwa katika CCM au hupo, una haki hiyo.
Sasa wazee wanapoanza kuzungumza kuhusu ‘utaratibu wetu’ miye naona kama vile wanataka kuwatisha wana CCM wenye nia ya kugombea cheo hicho.
Lakini, kuwania kiti chochote kile, ni haki ya kila mwananchi. Na wazee wangetusaidia sana kama wangeshikilia kuwa Katiba ifuatwe neno kwa neno, na siyo kusema mambo yaendelee kama ‘enzi zetu’.
Kwa heshima na taadhima, sharti tuwaambie wazee wetu kwamba wanapswa kutambua kuwa hizi ni nyakati zingine. Enzi zao, ‘Enzi za Mwalimu’, kuwa kiongozi katika CCM lilikuwa ni jambo la kujivunia na kuheshimika.
Leo je?
Yaani, wazee wanataka kutuambia mikiki iliyokikumba Chama chao ni uongo? Kama ni hivyo, basi Watanzania tutakuwa wanafiki wa kutisha. Inabidi tuwaeleze wazee wetu, wajue kuwa sasa wananchi tumefanywa mafala na mibwege ya kutupa. Ila, wakati umefika wa kusema kuwa hatutakubali kuendelea kupuuzwa namna hii!
Hata vijana na makada wao wa chama wamechoka na wanakerwa sana. Mbunge wa Kishapu (CCM), Fred Mpendazoe, amesema kuwa ni lazima wananchi wote, bila kujali itikadi zao, washikamane kupambana na mafisadi ambao alisema ndio wanaoitafuna nchi peke yao.
Mpendazoe amesema wazi-wazi kwamba, wananchi hawataielewa serikali yao iwapo haitawachukulia hatua wamiliki wa kampuni ya Kagoda Agricultural Limited inayotajwa kuwa imechota mamilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ilyokuwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, na kashfa nyinginezo.
Wazee wameonyesha kukerwa na tuhuma za ufisadi zinazoelekezwa kwa baadhi ya wana CCM wenzao. Sasa wazee wetu wanataka nini? Tujifanye kuwa huo siyo ukweli bali ndoto za mwendawazimu tu?
Nao akina Mpendanzoe na makada wenzake kadhaa katika CCM wameonyesha kukerwa na tabia za kuendelea kuwakumbatia watuhumiwa wa ufisadi wakiwemo na wizi wa fedha za EPA.
“Kuna methali ya Kisambaa isemayo: Ukitaka kuepukana na nzi, tupa mbali kibudu. Hii ina maana kwamba ukitaka kuepukana na harufu chafu, using’ng’anie mzoga,” alisema Mpendazoe.
Labda wengine wangemuuliza Mbunge huyo: Je, kama wewe ni fisi, kweli utaucha mzoga huo? Kwa fisi, kwake kila kitu anaona mambo poa tu!

No comments: