Saturday, July 18, 2009

Wasiotaja mali watavuliwa ubunge?

Sidhani kama kuna kiongozi yo yote amewahi kutaja mali alizokuwa nazo na madeni yake. Yanakuwa mavungo tu. Labda hayati Mwalimu Nyerere.

Kwanza tangu uhuru hakuna kiongozi yo yote ambaye ameulizwa kuwa imekuwaje ghafla amekuwa tajiri. Siyo tabia na utamaduni wa Bongo. Mara nyingi ni wizi tu, lakini utamaduni wetu ni kuwa sisi tunasifu wezi.

Mimi nadhani hata hizi shuku za ufisadi wa hali ya juu uliofanyika. Haya yatakwisha hivi hivi. Wakuu wanafikiria mambo haya yatasahaulika na tutaendelea na porojo kibao. We anzisha tume fulani halafu wakileta uchunguzi wao, weka hilo faili kabatini. Imetoka hiyo!

Lakini upo mwisho wake juu ya kuwa.Watanzania tunaonekana siyo wachovu wa porojo. Sasa naona Spika wa Bunge Samwel Sitta amewatahadharisha wabunge kuwa mwaka huu atakuwa mkali na kuwachukulia hatua za kisheria watakaochelewesha kujaza na kurejesha fomu za kutaja mali na madeni yao.

Mimi binafsi siamini. Tangu uhuru, nani kachukuliwa hatua za kisheria kutajirika ghafla baada ya kupata utajiri wa ghafla?Kuna jambo la kuoneana aibu kwa uongozi katika awamu zote tangu tuanze kujitawala – au tangu kuanza kwa ukoloni mamboleo ambao tunao sasa.

Katika awamu ya kwanza wezi wa kutumia ofisi zao walikuwa wanajificha nyuma ya ndugu zao. Ulikuwa unaona ofisa anaendesha kagari feki kweli, lakini ni milionea, tena mzito.

Hivi leo kwa nini wabunge wasifanye hivyo hivyo? Tunajua Bunge letu limenunuliwa na wenye fedha. Sasa wanaanza kujiandika kazi katika nyadhifa mbali mbali za serikali kusudi kuvuna faida ya ya mtaji walioweka.

Kwani kuna kazi gani kuanzisha kampuni na kuandika majina ya wakurugenzi kama ifuatavyo; Mkurugenzi mkuu- Adam Lusekelo. Wajumbe wa bodi ni Lusekelo Adam, Njinja Maloni, Asumani Mwanjotile, Mama Chale na Bi Chiku ambao wote ma-besti wangu?

Unampelekea hiyo fomu bwana Spika naye ataridhika na kusema kuwa bwana Lusekelo ametaja mali alizokuwa nazo! Masiala hayo! Naona wangetumia karatasi za fomu hizo kwa manufaa zaidi – kama kuwapa waheshimiwa wa mahakama kuandikia. Nasikia mahakama zingine hazina karatasi za kuandikia.

Tutake tusitake, baado utamaduni tuliojenga ni wa kusifu wanyang’anyi wasiokua na silaha, wenye kuvaa suti na kuendesha magari ya fahari, na wenye ku-rap katika kila kumbi kuwa nchi yetu ni masikini.
Kuna njemba moja (Mkurugenzi wa Kampuni ya umma) aliambiwa ataje mali zake na washiriki wake katika kampuni hiyo. Basi alitia jina la mke wake, na wakurugenzi wanne, ambao baadaye ilijulikana kuwa ni watoto wake. Mkurungenzi wa mwisho alikuwa baado anavaa nepi! Bwana Spika ana kazi

No comments: