Tuesday, July 7, 2009

Chombezo la Adam Lusekelo

Alivyokuwa aki-rap kwenye mkutano wa CCM huko Dodoma, mwenyekiti wa chama aligusia vyombo vya habari. Siasa za kuchafuana zimeshamiri hapa nchini.

Pia alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari kuwa vinatumia vibaya uhuru wa habari kwa sababu za kisiasa. Aliongeza kuwa , ipo minong’ono kuwa uhuru wa habari unatumika vibaya baada ya kuchukua kitu kidogo.

“Uhuru wa vyombo vya habari umekuwa ukitumika vibaya kwa baadhi ya vyombo vya habari kwa sababu ya kisiasa, kutompenda mtu. Kuna fununu kwamba vipo vyombo vya habari ambavyo hupewa kitu kidogo kufanya kazi hiyo. Hawa nawaomba wazingatie maadili ya kazi zao ili wautumie uhuru huo vizuri.” Ali-rap mwenyekiti huyo.

Sawa kabisa. Kazi yetu ya uandishi wa habari unazungumziwa sana, hasa na wanasiasa. Tunatakiwa tuandike ‘vizuri’, na tusichafulie watu majina. Tupambe. Ukisikia ‘tusichafulie watu’ ina maana ‘tusiwachafulie wanasiasa majina.

Mimi naona na sisi vyombo vya habari tuitwe Kizota, huko Dodoma. Tukafanyiwe semina kuelezwa tuandike nini hasa ambavyo vitawaonyesha ndugu zetu wanasiasa kuwa tunaandika ‘vizuri’?


Turudi nyuma kidogo tu. Wakati wa kampeni wa uchanguzi mkuu, wanasiasa waliwaandika kazi waandishi fulani wa habari, ili waripoti kila watakachofanya, isipokuwa labda kwenda chooni na wakiwa na hawara zao. Sisi wenyewe tunajuana sana.

Jobu hilo linafanywa hata leo. Na litazidi tukiingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, Na nakubali kuwa kweli kuna baadhi yetu ni mazanga tu wanaotumia uandishi wa habari kujinadi kwa bwana ye yote atakayetoa vijisenti.

Mradi utumbo aliosema fulani utoke kwenye gazeti, TV, redio au sehemu zingine za vyombo vya habari. Mimi ninajua kuna watu wengine,hasa wanasiasa wanaopigia simu vyumba vya habari na kuuliza kwa nini utumbo waliosema siku kadhaa zilizopita hazikuchapishwa.

Lakini pia kuna mambo mengine hayakwepeki. Baado nchi inangoja kujua nini hasa kilitokea katika kashfa ya Richmond? Je mkataba wa Buzwagi kwenda kusainiwa Uingereza. Nini tena? Na mahela ya Benki Kuu je? Huko ni kuchafulia watu majina? Hii ni nchi yetu wote na siku hizi huwezi kujifanya unajificha. Watu watajua tu!

Kama mtu ana-swing na mke wa mwenzake tutajua tu. Huko siyo kuchafuliana majina. Kama kuna mchiki ambaye anajiuza ili apate feva fulani kiofisi au kisiasa, tutajua tu.

Kama kuna mtu mwizi kiofisi au kishirika itajulikana. Majitu wenyewe hayawezi hata kuficha hizo fedha walizoiba. Maana sisi hatuna utamaduni wa kuwa na fedha nyingi. Mtu aliyetoka kwenye kibanda cha nyasi akiiba vijifedha kidogo, utamuona tu.

Atataka kila mwanamke awe wake. Atataka magari mengi ya fahari. Atajenga jumba utafikiria yeye na mkewe wanataka kucheza tennis ndani ya jumba hilo

Mkuu amesema baadhi ya waandishi wamepewa kitu kidogo. Na ikigungulika kuwa baadhi ya wana siasa wamepewa makitu makubwa, kama mabilioni ya fedha, tukae kimya?

Waandishi na wanasiasa ni paka na panya. Hawawivi. Baadhi ya wana siasa wana mengi ya kuficha, pamoja na ufisadi. Kazi ya vyombo vya habari ni kifichua madhambi hayo na kuwaambia wananchi nchi yao inavyobakwa. Huko siyo kuchafulia watu majina.

Mwendawazimu akibaka kasichana ka miaka sita, tutasema. Na pia mwanasiasa akiibaka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuiibia mabilioni pia tutasema! Hatuwezi kukaa kimya, eti sababu kavaas suti. Situ ni vazi ambalo majambazi pia yanaweza kuvaa
!

No comments: