Tanzania watawala kibao - viongozi kau
Hivi majuzi Waziri Mkuu, Braza Mizengo Pinda alisema kuwa nchi inahitaji viongozi wasukuma maendeleo ambao wanakerwa na matatizo ya wananchi, badala ya watawala.
Braza Pinda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watawala wanaojiita viongozi na wawakilishi wa sekta mbalimbali za jamii wakiwamo wa dini katika halmashauri za Kasulu na Kibondo mkoani Kigoma.
Alisema kuwa anakerwa na watendaji ambao wanakaa ofisini bila ya kuwafuata wananchi na kuwastua juu ya fursa zilizopo, ambazo zinaweza kuwainua kiuchumi.
Sisi wananchi tunajua fika kuwa sasa hivi kuna makatuni lukuki ambao wanajifanya ni viongozi, utafikiria uongozi ni kazi rahisi! Wengi wanakuwa kama watoto vile, kupoteza muda mwingi kutafuta midoli ya kuchezea, kama magari ya kifahari na kujikita katika mbwembwe mpaka wanatia huruma.
Nasema hivyo, kwa kuwa nina mifano mingi, hasa nje ya jiji la Dar es Salaam. Ukienda huko mikoani na wilayani, utaona watu wanasimama eti pale mkuu wa wilaya au mkoa anapoingia baa. Mimi naona uchizi huo; usiniambie ni heshima kwa mkuu. Ni uoga tu usiokuwa na msingi!
Lakini huwezi kumlaumu mtawala huyo sana. Wa kulaumiwa pia ni wananchi wanaofanya hivyo. Kumtukuza binadamu mwenzio kana kwamba yu Mungu-mtu kuna hatari sana. Baada ya muda, yawezekana akaanza kuamini kuwa yeye kweli ni mungu mtu, wa kupapatikiwa na kila mtu!
Mtawala mmoja, yeye ni waziri na ushahidi ninao, alikuwa anawasili mjini Dar es Salaam kwa ndege. Sasa dereva wake alikuja kumpokea kiwanja cha ndege. Dareva huyo aliacha shangingi la mkuu, likinguruma ili kiyoyozi ndani ya shangingi hilo kiendelee kufanya kazi!
Gari tupu, hamna mtu ndani, linanguruma kumngoja waziri ambaye ndege aliyokuwa amepanda hata haujatua. Dereva wa gari hiyo alikuwa amesimama pembeni na mwenye sura kama aliyekuwa anamngoja Mwenyezi Mungu mwenyewe afike.
Ni dhahiri kuwa dereva huyo alikuwa anafanya hivyo kwa amri ya mkuu. Waziri huyo anajiita profesa, lakini kwangu mimi ni katuni limbukeni tu. Ni dhahiri kuwa shule yake haikumsaidia sana. Angekuwa analipia mafuta ya gari hilo kutoka mfukoni mwake angethubutu kuamuru libaki bila kuzimwa muda wote?
Kwan nchi masikini kama yetu, kule tu kuwa na mashangingi, ni matusi kwa wananchi. Kuna magari mengi yanayoweza kufanya kazi ya mashangingi. Kwa kukubali ukatuni huyo, serikali inatueleza kwa vitendo, bila kusema, inavyotufikiria sisi wananchi. Unaenda baa na watoto wako hawajala!
Pia kuna uonezi kibao mikoani. Braza Pinda, angepitisha upekuzi wa kimya-kimya huko na kuona jinsi watu wanavyoonewa. Inakuwaje mkuu wa mkoa au wa wilaya awe na utajiri mkubwa ghafla mara tu baada ya kutinga katika kituo chake?
Kwa mfano, katika mkoa fulani wa kusini mwa Jamhuri yetu, watu walistukia ghafla mkuu wa mkoa huo tayari ana maelfu ya ekari, na analima ngano! Wakati wa kuvuna alikuwa akibeba ngano hiyo kutumia magari ya serikali. Sasa hivi ni milionea na hana wasiwasi. Lakini maelfu ya eka za mashamba ya ngano katoa wapi kama siyo kutumia ofisi yake vibaya?
Sasa, kama mkuu wa wilaya na afisa kilimo na kila ka-jiofisa, wote watafanya hivyo hivyo, si ndiyo basi, nchi inakuwa haina viongozi tena, bali watawala? Matatizo yetu Waafrika ni kuwa, tunajaribu sana kukimbia zile tembe za nyasi tulizokulia. Gari moja halitoshi, labda manne, ya nguvu! Nyumba moja ya kawaida haitoshi, mpaka liwe hekalu. Sasa, hiyo si njaa tena, bali uroho!
Kiongozi anatakiwa kuongoza, ili sisi wengine na watoto wetu tuige mfano wao. Wananchi hawawezi kuiga mfano wa watu waroho. Hao siyo viongozi. Hao ni watawala wa kudharauliwa na kuonewa huruma kwani matatizo yao ni ya kisaikolojia!
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA CMA KWA UANZISHWAJI WA MFUMO WA KIDIJITALI.
-
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa uanzishwaji wa Mfumo wa Uendeshaji na
Us...
8 hours ago
1 comment:
I KNEW YOU GONNA DO THIS. NASEMA BRAVO THOUSAND TIMES FOR DOING THIS. HOLD THEM ACCOUNTABLE NA WALA USIOGOPE. WE NEED A STONG CIVIL SOCIETY, AND YOUR NUMBER ONE. WAKATI UMEFIKA WA KUWAAMSHA NA KUWAKUMBUSHA WANANCHI ILI WATUMIE NGUVU YAO YA KURA KUWATIA NIDHAMU VIONGOZI WAZEMBE, WAVIVU, WABINAFSI, NA WALARUSHWA. DON'T LET THEM PLAY YOU FOR A SUCKA. IF YOUR MBUNGE PROMISSED YOU MORE TEACHERS, FIGHT AGAINTS UNEMPLOYMENT, AND BETTER ROAD CONDITION IN YOUR AREA, AND HE DIDN'T DELIVER, PLEASE ASK HIM/HER WHY. KAMA HAURIDHIKI NA MAJIBU YAKE DON'T VOTE FOR HIM. ELECT SOMEONE ELSE. OUR GOVT AND LEAERS HAVE LET US DOWN GAIN AND AGAIN AND AGAIN. ENOUGH IS ENOUGH. TUKITUMIA KURA ZETU VIZURI TUTAWEZA KUBADILISHA MWELEKEO WA MAISHA NA NCHI YETU.
Post a Comment