Friday, May 29, 2009

Mwanadamu na uroho

Nilikuwa naviangalia vitoto vinacheza, kitu ambacho nainjoi sana. Mtoto hana aibu. Kila kitu wanachokiona wanataka kiwe chake. “Hii yangu! Hii yangu. Gari yangu!”

Huo ndiyo utoto. Lakini baada ya kufikiria kidogo nikagundua kuwa utoto ndani yetu haututoki, hata tukikua kiumri. Bado utakuta watu wazima wanaendelea na ‘hii yangu!’ mpaka waende kwa aliyewaumba. Sasa unaiba mabilioni ili iwe nini?

Karibu kila siku utakuta magazeti yanalia kuhusu rushwa nchi yetu. Dini zote kubwa na ndogo zinazungumza kuhusu kiasi. Sisi Bongo hatuna kiasi-ni kunyang’anya kila kitu.

Nilivyokua ughaibuni nilisoma kuhusu kijana wa miaka 27 ayekuwa anauza maziwa. Yeye alipata bahati nasibu na kushinda pauni milioni 15 za kiingereza. Kwa leo pauni moja ni sawa na shilling 2,000 za Bongo. Fanya hesabu mwenyewe.

Waandishi walivyomuhoji kijana huyo alisema kuwa amegundua kuwa juu ya kuwa na mamilioni hayo bado anakunywa vikombe viwili tu vya chai asubuhi na slesi za tosti mbili na siku nyingine na yai moja la kuchemsha. “Huwezi kula sahani kumi za mlo kwa ajili wewe ni milionea.” Alisema.

Haya, sasa yeye alishinda. Hapa Bongo hakuna hiyo. Ni watu kuiba kwa kutumia ofisi za wananchi wa Tanzania. Na hawawekwi hatiani. Si ajabu wanapewa vyeo zaidi. Hawa mabraza baado wanafikiria wanaweza kula sahani ishirini za mloo kwa kikao kimoja.

Kumbuka ni utoto ule ule wa ‘hii yangu!’ Wewe utapanda magari mangapi. Unakuta njemba ina magari 12 katika ua wake. Unaikuta njemba ina nyumba tano Dar, tano Arusha, flati mbili London.

Lakini hata ufanye nini, utalala kwenye chumba kimoja tu, na kitanda kimoja. Utakuwa na mchiki mmoja kwa wakati mmoja. Najua kuna mtawala mmoja huko Africa Magharibi aliyechukua machiki wanne kwa wakati mmoja. Akameza na vidonge sita vya Viagra vimsaidie nguvu za kiume. Kesho yake alikutwa amekufa. Uroho huo!

Watu matajiri wenye fedha wamegundua ubaya wa uroho na kujilimbikizia marundo ya fedha. Bill Gates ametoa dola million 25 kusaidia mapambano dhidi ya gonjwa la malaria linaloua mamilioni kila mwaka. Marehemu Carnegie wa umarekani aliamuru utajiri wake utumike kuanzisha maktaba katika nchi zote zinazoendelea.

Na hao wamepata utajiri wao kwa halali, siyo kwa kuwaibia wananchi wao. Siyo kama majambazi wetu wasiokuwa na silaha na wanaovaa siti, wasiojua neno ‘kiasi’ “Hii yangu!”

Lakini Mwenyezi Mungu ana breki zake kiboko. Ameamua hata mtu uibe vipi akikuchukua utaenda peke yako. Yale mashangingi uliyoiba hapa hayatoshi kuingia katika kaburi lako. Ule mlima wa vitu uliliokuwa unakusanya wakati unawaibia wananchi hautoshi kaburini. Utaviacha vyote hapa hapa!

Mafirauni ambao walitawala Misri zamani za kale walijaribu kwenda navyo vitu peponi, pamoja na watumwa. Wao wameudedi miaka elfu tatu iliyopita. Itakuwa mafirauni wa leo?

Sasa leo tunawaangalia watu wanaofikiri wataishi milele. Inanikumbusha vile vitoto vinavyosema ‘Hii yangu!’ Ni uroho tu. Hawakui!

1 comment:

Anonymous said...

Nimgetamani watawala wetu wawe wanazingatia haya unayoandika lakini wao hujiona wateule na wanahusudu msemo wa PONDA MALI KUFA KWAJA.