Friday, September 11, 2009

Chombezo la Adam Lusekelo

Aliyekuwa Rais wa nchi ya Peru, Marekani ya Kusini, Alberto Fujimori amebamizwa lupango miaka sita – kuna kesi zingine zinakuja. Amehukumiwa hivyo kwa kutumia vibaya madaraka.

Mpaka sasa tunadhani hayo hayawezi kutokea Bongo. Lakini huko ni kudhani tu. Yatatokea siku moja. Lazima tuanze kuulizana maswali. Siyo watu wanaapa kuitumikia nchi yao kwa uadilifu halafu wanaanza ufisadi na uonevu wa watu wao na kuuza nchi yao kipande hadi kipande.

Fujimori pia alikabiliwa na mashitaka ya kuteka nyara maadui wake, ufisadi na hata kutoa amri ya kuua kwa watu waliokuwa wakimpinga kisiasa. Akipatikana na hatia anaweza kupumzika lupango kwa miaka hadi 30.

Mbabe huyo alikuwa akitawala nchi hiyo ya Peru kama shamba lake binafsi. Kwanza wananchi walivyopamba moto alikimbilia Japan ambako ukoo wake ulitokea. Lakini alivyorudi marekani ya kusini tu alirudishwa Peru, na hatimaye alipelekwa kortini na sasa yuko lupango.

Sawa kabisa! Ni kwamba haiwezekani mijambazi miongo ikajiingiza katika siasa za nchi kilaghai na kuapa itawatumikia wananchi wa Tanzania. Ikishapata hizo ofisi, mara nyingi kwa kununua kura au kuhonga, inaiba kifashisti!

Halafu kuna kulindana sana, nchi hii. Naambiwa kuwa miaka mitatu hii watu walikuwa wanalipa fadhila kwa watu waliochangia katika uchaguzi uliopita. Mimi siiti kuchangia, naita magendo. Kuhonga. Unahonga chama tawala, kinakupa ofisi halafu unaanza kuiba kama huna akili nzuri.

Sijui jamaa hawa wanatuona sisi mimbunju? Wanatuona sisi mabwege kweli kweli! Mafala wa kutupa! Na mwisho ya yote – tutawafanya nini? Wao wana mabunduki.

Ukihutubia wananchi unakuwa umezunkukwa na FFU wenye urefu wa futi nane, wameshika mabunduki na marungu. Nani atafanya fyoko?

Lakini dikteta Ferdinad Marcos wa Ufilipino pia alikuwa na askari wa kuzuia fujo wenye futi nane, mabunduki na marungu. Lakini wananchi wakamwambia aambae tu. Mwisho nchi ikawa haitawaliki.

Mwisho bwana Marcos akaita jeshi. Wanajeshi wakaja na mabunduki na vifaru na sura za kibaghaili kweli. Wananchi hawakujali. Eti jeshi lilioloapa kulinda mipaka ya nchi linatumiwa kuwatishia wananchi. Watu wakawazomea na kuwaambia wawauwe tu.

Masista wakawa wanazunguka vufaru hivyo na kuweka mauwa kwenye mitutu ya mabunduki ya wanajeshi hao. Askari wakaanza kuona nishai- utapigaje risasi masista? Marcos akaachia ngazi.

Hapa Afrika Frederick Chiluba alijiona mjanja huko Zambia. Ufisadi huo huo. Alijifanya kaokoka. Katika mlokole huyo hakuona kibaya akiiba dola 48 milioni za waZambia. Na hakuamini alipovishwa pingu na kupelekwa mahakamani! Aliyekuwa mbabe huyo sasa ana ugonjwa wa presha kali na wasiwasi. Inabidi kila wakati apelekwa kutibiwa huko Afrika Kusini,

Bongo jamaa wametulia tuli - wanauza nchi tu. Tutawafanya nini? Sisi wananchi tunafanywa mibwege. Lakini iko siku tutaanza kuulizana maswali.

No comments: