Tuesday, October 13, 2009

Ni haki tu,wauaji wanyongwe

Unajua, kuna kitu ambacho kinamfanya mwanadamu kuitwa mwanadamu. Pamoja na kutembelea miguu miwili, hisia zote na kubwa zaidi akili. Hiyo ndiyo inamfanya mwanadamu ajitenganishe na viumbe vingine vya mwenyezi Mungu.


Kuna vitu vinavyofanya mwanaadam aitwe mwanadamu. Mtu anayeonekana kama mwanadamu, halafu akaishia kuwa na mwenendo wa kinyama mara nyingi hatusiti kumwita mnyama.

Sasa hivi karibu nchi nzima imekumbwa na mjadala mkali baada ya watatu watatu kuhukumiwa kunyongwa kwa kumuua kijana, Masumbuko Dunia (13) ambaye alikuwa ni mlemavu wa ngozi.

Jaji Gabriel Rwakibalila aliwakuta vijana hao watatu, mjini Kahama, na hatia ya jinai ya kuua kijana huyo kwa sababu za kishirikina. Eti kupata viungo vya vya kijana huyo, au mtu yo yote mwernye ulemavu wa ngozi kutawawezesha kupata utajiri. Sasa kuna wanaopinga hukumu ya hiyo ya kifo.

Wanataka kuwafanananisha wauaji hao na watu wa kawaida. Lakini wote tunajua hivyo sivyo. Watu watatu wakikaa na kupanga mauaji ya kinyama (pre-meditated murder) ya mwanadamu mwenzao, ili kumkata kata viungo vyake, ili waviuze, ili wawe matajiri, si watu hao, ni wanyama.

Simba mla watu akiua wanavijiji, hakuna mtu anamuonea huruma. Serikali inawatuma ma-game ranger, ili kumuua simba huyo. Hakuna mtu anayeshituka. Kwanza ndiyo jamii inashukuru kuondolewa na kero hiyo ya hatari.

Afadhali hata simba, anayeuwa kwa ajili ya njaa. Hayo majambazi, yanayo jiita wanadamu, hayakua na nia nyimgine bali uroho wa kinyama na ushirikina. Yanatisha jamii, kama vile simba mla watu. Sasa kwa nini jamii isijikinge na wanyama hao, ambao wanatumia akili zao kuwinda binadamu wenzao kama wanyama?

Jamii ina haki kabisa ya kujihami. Wasingekamatwa na vyombo vya dola
nina hakika wangaeendelea na uovu wao wa kutisha. Kwa nini waachiwe waendelee kukera jamii?

Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema kuwa hoja isiwe jino kwa jino bali kutovunja haki za binadamu. Mimi nadhani mtazamo huu unapakwa rangi kidogo na mafundisho ya dini. Kusamehe.

Kama ni haki za binadamu, mbona majambazi hayo hayakufikiria kuhusu haki za kijana Masumbuko Dunia? Wakamchinja kama mbuzi, halafu tukae nao katika jamii? Hiyo haiendi kabisa.

Wanasema kuwa adhabu ingefaa kwa kuwarundika ndani ili wajirudi. Je aliyeuawea anajirudi vipi. Tena, swala hapa siyo wao majambazi. Swala ni jamii ambayo inalazimishwa kujikinga na ugaidi wa wanyama hao wanaojiita watu.

Wanaotetea wanyama hao wa Kahama wajiulize – je , ingekuwa aliyeuawa na kukatwa katwa vipande kama mbuzi angekuwa mwanao ungefanya nini? Ungesema afungwe na kupewa nafasi ya kujirudi, ili asiuwe watu wengine?

Nasema tena, jamii ina haki ya kujikinga na kuwaondoa wanyama hao kabisa. Na hilo liwe onyo. Mimi naona tusipoteze hata muda kwa kulumbana kuhusu ‘haki’ za wanyama hao. Kama hawakuweza kuishi katika jamii na kudhalilisha jamii nzima, basi wanyongwe tu

Wauaji hao wametangaza vita dhidi ya jamii. Sasa katika vita watu wengi wanageuka kuwa wanyama. Ndiyo maana mahakama za wakati kama huo hutoa adhabu ya kifo kama ni onyo la waharibifu. Majasusi na wahaini hunyongwa. Na wauaji, kwa sababu usalama wa nchi unakuwa siyo makini, wakipatwa wananyongwa. Haki za binadamu? Na haki za raia je?

Huwezi kusema ukarejesha wanyama kama hawa kwenye maadili na utu. Wakionja damu ya mtu huwezi kuwarudisha katika mabadiliko katika maisha. Eti wauaji wanaweza kuwa mfano mkuu wa jamii na kufanya watu wengi kukiri udhaifu wao na kuwa wanyoofu maishani. Kusadikika huko!

No comments: