Saturday, October 31, 2009

Hawa ni majizi tu!

Katika kumbukumbu ya mzee wetu, Mwalimu Nyerere, aliyetutoka miaka kumi iliyopita wengi wetu tumekuwa tukilaani hali tuliyonayo nchini, kwa kijanja sana. Karibu kila mtu anasema - Enzi za Mwalimu…

Kusema hicho wakati tukimkumbuka, imekuwa ni kama watoto waliobakizwa yatima. Lakini kikubwa zaidi ni kuwa tumewahi kuwa naye na sasa tunalaani tawala zilizofuata kwa kujifanya kumsifu na kumuenzi Mzee.

Sasa kama watu wakimuenzi marehemu baba yako na kutosema lolote kuhusu wewe mwenyewe, basi ujue wanakuponda kiungwana. Wengi wametumia nafasi hii kuponda yaliopo.

Nimewahi kuishi katika nchi jirani,Kenya, kwa miaka mitatu. Nimeona wenzetu wakisema ‘uzalendo’, wao wana maana binafsi. Ndugu zetu walipambana na wakoloni wa Kiingereza huku wakijifikiria wao binafsi. Wakina Lord Delamare na wakoloni wengine walivyong’olewa, waliokuwa wanajiita wazalendo waliingia kwenye utawala na kufanya madudu zaidi ya wakolini wenyewe.

Niliona shamba la aliyekuwa rais, Mzee jomo Kenyatta kati ya barabara ya Nairobi na Nakuru. Kulia ni shamba la Mzee na kushoto shamba la Binti yake, Margaret Kenyatta. Kwa kifupi tu – ni kufuru.

Na usiambiwe, kelele zote kutoka kwa jirani zetu ni hasa kwa sababu hawana ardhi. Ardhi yote imenyakuliwa na wajanja na watawala. Wananchi walio wengi wanakaa katika mageto, wao wanaita rizavu (native reserves) mijini.

Biashara zote kubwa zilikuwa na ni za familia na rafiki zake. Mpaka sasa imekubalika, au inaonekana hivyo. Majizi yamekubalika tangu walipopata uhuru.

Tanzania tuna mfano tofauti. Tulipata kiongozi na wenzake waliyeongoza nchi. Siyo kikundi cha watawala ambao wanafikiria kazi yao ni wizi.

Ukifananisha na yaliofuata utamfanya Mzee Nyerere awe ni mtakatifu. Ukifananisha na majambazi, kama Mobutu wa iliyokuwa Zaire (DRC), Omar Bongo (Gabon), Mugabe ambaye anaiga Kenya, utamuona Mzee Nyerere ni tofauti kabisa. Kwake nchi ilikuja namba moja. Uzalendo.

Mwalimu kaondoka na sasa tumebakia na unafiki wa kutisha. Eti, majitu yanauza nchi, na yanasema yanafuata maadili ya Mwalimu.

Huu unyang’anyi wa rasilmali za taifa zisiusishwe hata kidogo na hayati Mwalimu. Huu ubinafsishwaji na wizi wa viwanda vya umma uwekwe mbali kabisa na Mwalimu. Majambazi yameuza nchi na tuyaite hivyo hivyo – majambazi.

Mafisadi tuwaite hivyo hivyo – majizi, hakuna kuanza kuwapaka wanja watu wanaotia kichefu chefu. Hivi sasa dhamira ya kutumikia umma ni ndoto. Uongozi kwapu kwapu ndiyo unatamba.

Shukrani moja kwa Mwalimu ni kuwa alituachia kipimo cha maana ya uongozi. Kwa hiyo kila mwaka kumbu kumbu ya kututoka kwake uwe ni wa kuyazomea majizi na majambazi hayo.

Mambo yanayotokea sasa ya kuuza (wao wanaita lease) ardhi, kama wale machifu wa karne iliyopita yaandikwe vizuri kabisa. Machifu hao waliuza ardhi ya Tanganyika ili kupata shanga za wake zao, ulevi kama whiski, na kaniki. Majina ya machifu wa leo yaandikwe na kumulikwa vizuri ili wajukuu na vitukuu vyao wajue kuwa mababu zao walikuwa ni wahaini wakubwa wa nchi hii nzuri.
Nionavyo mimi katika ujambazi unaoendelea hivi sasa, Hayati Mwalimu Nyerere ataendelea kuwa mioyoni mwetu. Na kwa majambazi na majizi yanayoendelea ni kuwa wananchi wa Tanzania wana mfano wa kuwafananisha nao. Huu uovu hautaruhusiwa kuendelea milele. Mwalimu katutoka. Lakini Mwalimu bado anaishi!

No comments: