Majizi yafungwe kwanza kabla ya Marshal Plan
Wakati wa Mkutano wa Leon Sullivan mwaka mmoja uliopita kulikuwa na maneno ya kututia moyo sisi Wafrika katika mkutano wa Leon Sullivan unaoendelea huko Arusha. Binafsi nilipendezwa sana na maneno ya rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na mchungaji na mwanasiasa maarufu wa Marekani, Jesse Jackson.
Jesse Jackson amekuwa na maoni kwamba ili kuiwezesha Africa kupata maendeleo ya haraka lazima jamii ya kimataifa, kwa makusudi, ibuni Marshal Plan kwa ajili ya Africa.
Sasa Marshal Plan ilifanywa na Umarekani kwa nchi za ulaya ziinuke kiuchumi baada ya kuteketezana katika vita vya pili vya dunia vya mwaka 1939 hadi 1945. Na kweli iliwezekana. Ndiyo leo tunaiona ulaya ilivyoendelea.
Mchungaji Jackson ndiyo ameshauri hiyo. Na mimi nakubaliana naye. Lakini naona kwanza kabla la hilo tufuate ushauri wa Obasanjo kwanza.
Yeye alitoa kauli nzito dhidi ya viongozi wa Afrika na kuwataka kupambana na rushwa katika nchi zao, hata kama zinawahusu viongozi wakuu waliopo madarakani na wale waliostaafu ndani ya nchi zao.
“Ili mataifa ya Afrika yaweze kupata maendeleo lazima viongozi wake wakubali kupambana na wala rushwa katika nchi zao, hata kama ni wakuu ndani ya nchi zao,” alisisitiza Obasanjo.
Nasikia kauli hiyo ya Obasanjo ilisababisha ukumbi mzima wa AICC kupiga makofi na kumshangilia, kitendo ambacho kilionyesha jinsi suala la ufisadi linavyowakera wengi wa Waafrika.
Kutoka Tanzania na Afrika nzima, lazima tufikie mahali tuanze kuulizana maswali na tuone hatua zikichukuliwa. Mwizi ni mwizi tu! Hatuwezi kusema rais au aliyekuwa rais akiiba basi ni ‘mla rushwa’ na mwizi wa kuku au simu ya mkononi ni mwizi wa kuuawa.
Wote ni wezi tu na lazima wachukuliwe hatua. Hata siku moja mwizi asije akaniomba mimi nimheshimu. Mimi nitakaa naye mbali sana.
Maana yake sasa barani Afrika imekuwa utani. Mtu anagombea urais ili aende akafuje mali, aibe na ajinufaishe. Eti, anaenda Uwanja wa taifa, anashika msahafu na kuapa kwamba atawatumikia Watanzania kwa utii, uadilifu na uwezo wake wote. Anaomba Mwenyezi Mungu amsaidie!
Huko ni kumtania Mwenyezi Mungu! Kumbejeli na kumkebehi Mwenyezi Mungu. Tumekubaliana kitaifa viongozi watalindwa mpaka Mungu akiwachukua. Hawatakufa na njaa. Lakini uroho hauwaishi.
Najua sisi bianadamu tunatabia ya uroho. Lakini kama wenzetu wa nchi zilizoendelea wanachukuliana hatua pale pale mauroho yanavyo washinda, lazima na sisi WaAfrika tuweke mikakati kama hiyo.
Obasanjo alisema: “Inabidi tukubali na tuwe tayari kuwafikisha mahakamani hata mawaziri na wakuu wa polisi kama wamehusika na vitendo vya rushwa, ndipo tutaweza kujipanga na hatua nyingine ya kukuza uchumi wa nchi zetu.” Alisema Mzee Obasanjo.
Kauli hiyo ya Obasanjo imekuja wakati marais kadhaa wastaafu wa Afrika, akiwamo yeye mwenyewe, wakiwa wanatuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka walipokuwa viongozi.
Pamoja naye, orodha ya marais wastaafu wanaokabiliwa na tuhuma hizo ni pamoja na Benjamin Mkapa wa Tanzania, Frederick Chiluba wa Zambia na Bakili Muluzi wa Malawi.
Sawa kabisa. Nadhani JK amesikia vizuri sana kauli hiyo ya Obasanjo. Hakuna kitu kibaya sana kama wananchi kukosa imani na serikali yao!
Jirani zetu kama Zambia, Malawi wamaulizana maswali. Sisi tunangoja nini? Krismas?
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA CMA KWA UANZISHWAJI WA MFUMO WA KIDIJITALI.
-
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Tume
ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa uanzishwaji wa Mfumo wa Uendeshaji na
Us...
5 hours ago
No comments:
Post a Comment