Monday, June 22, 2009

CHOMBEZO LA ADAM LUSEKELO!!!!!

Kwanza nianze kueleza kabisa. Nikimwita kajambazi mwanafunzi wa Shule ya Pius Msekwa aliyemuuliza aliyekuwa Waziri Mkuu Lowassa Mkoani Mwanza namsifia. Ndiyo waTanzania tunaowataka. Wanaouliza maswali kama – kwa nini?

Alimuuliza mkuu kwa nini kauli za viongozi haziwiani na matendo yao. Na alimuuliza sababu za zilizomfanya rais ateue watu kama wabunge kuwa wakuu wa mikoa ilhali Bongo ikiwa na watu wengi wenye uwezo.

Namwita mwanafunzi huyo kajambazi. Kajambazi ka Bongo. Lakini nina maana mwanafunzi huyo ni shujaa. Ameuliza swali la akili. Nasikia vyombo vya usalama vilijaribu kumzonga mbavu. Siamini!

Mimi nafikiria kuwa vyombo vya usalama vina kazi muhimu zaidi kuliko kuwanyanyasa vijana wa kiTanzania wenye akili.

Nadhani vyombo hivyo vingemlinda sana mwanafunzi huyo. Ameonyesha kuwa bongo zimo ndani ya kichwa chake. Ningekuwa na fedha za kutosha ningekalipia hako kajambazi kenye akili mpaka kaende chuo kikuu. Ndiyo kitu tunachohitaji Tanzania. Bongo, na siyo wababaishaji

Kajambazi hako kalimuuliza waziri mkuu kuwa yeye na wasaidizi wake wanahimiza vijana kusoma kwa bidii na maarifa ili wawe viongozi wa taifa la kesho, lakini hawaoni hayo katika matendo yao. Lowassa alishindwa kujibu swali hilo.

Safi kabisa. Kajambazi hako kalikuwa kanasema mambo ambayo kila mtu mtaani anayasema. Mfano mimi. Nilimuona Hayati Mzee Nyerere nikiwa darasa la tatu. Mzee alikuja kwenye Open Day yetu, katika shule ya msingi ya Salvatorian, huko Kurasini, Dar es salaam.

Mzee alituambia kuwa sisi ni taifa la kesho. Poa kabisa. Tukaenda sekondari, mpaka chuo kikuu. Tulikuwa bado tunaaambiwa sisi ni taifa la kesho. Mzee ang’atuka na kurudi Butiama. Mpaka tukamzika Mzee wetu.

Baado kuna njemba zilizokuwa awamu ya kwanza, leo zipo. Awamu ya pili na njemba bado zipo. Awamu ya tatu. – njembist bado zipo. Na sasa awamu ya nne – njemba baado zinadunda tu! Aaa-a-a-a-h, masihara hayo!

Kama kajambazi kalivyokuwa kanasema haiwezekani kuwa mtu mmoja anakuwa kila kitu, Mbunge,Legino Kamishna, mwanyekiti wa Bodi ya Shirika la ndege la Tanzania, Msaidizi Kuu wa Chuo na mjumbe wa CCM NEC. Utani huo!

Leo mimi na uzao wangu kichwani mvi kibao – baado minjemba mingine imeezeeka na inatuambia sisi ni taifa la kesho. Jamani kesho hiyo ni ya lini? Watu tumekuwa! Tumeoa! Tumeachwa! Tumeoa tena! Tumejukuu! Baado tunaambiwa sisi ni taifa la kesho. Kesho ni lini? Eti mpaka ujipendekeze. Wengine mama zetu walitufunda na kutuasa tusijipendekeze.

Nadhani hawa wajomba wanaotutawala hawaelewi. Juu ya kuwa wanaweza kuchagua washikaji kwenye utawala, wananchi pia wanataka mabadiliko. Siyo Tanzania tu. Nchi zote ulimwenguni watu anachoka kuona sura zile zile kila siku.

Kale kajambazi ka shule ya sekondari ya Pius Msekwa kamesema kweli na kalindwe. Haiwezekani kuwa katika nchi ya watu 40 milioni na kuzidi mtu mmoja atakuwa na vyeo lukuki. Waziri yeye, Legino yeye,mbunge yeye, mwenyekiti wa bodi za wakurugenzi tatu ni yeye, mkurugenzi wa wachunga mbuzi wa Tanzania ni yeye. Utani huo!

No comments: