Saturday, June 6, 2009

Urafiki wa mashaka!

Siku mbili tatu zimepita nimekuwa nasoma soma makala kadhaa kutoka nchi jirani (kaskazini) Watawala wetu wamekuwa wakijifanya wanapendana sana. Ghafla wengine wamesema tuharakishe kutengeneza jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mimi nashangaa sana. Sijui ndiyo siasa hiyo au utumbo gani unafanyika. Wenzetu wanataka ardhi ya Tanzania. Eti mtu yeyote Afrika Mashariki aweze kukaa katika nchi yoyote. Eti tutumie vitambulisho tu na hamna haja ya pasipoti.

Unajua hakuna dharau kubwa kama mtu akikufanya bwege. Wenzetu Kenya wamekuwa wakitufanya mabwege, na sisi tumekaa kimya tu. Eti tuko waungwana.

Wana makala wa nchi jirani wamekuwa wakitutukana sana. Sasa ni muda wa kuwaambia Kenya waambae zao. Waache kabisa kutufanya Watanzania mafala.

Ukweli ni kuwa kwa wenzetu ardhi wamejigawia wakoloni wao weusi. Wakubwa kuwa na eka 500,000 za ardhi si kitu cha kushangaza sana. Uchoyo huo umewaondoa mamilioni kukaa mijini na ardhi haipo tena. Kaskazini ya nchini yao ni jangwa.

Sasa wamekuwa wakiinyemelea ardhi ya Tanzania kwa miaka mingi. Wanataka uchumba, tena uchumba wenyewe kwa nguvu. Jamaa hawajui hata kubonga!

Sasa wanatishia kuwa kama Tanzania haitaki kuingia Jumuiya hiyo, basi wengine, ikimaanisha Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi waendelee.

Mimi na Watanzania wengi tunakubaliana. Wacha Kenya Uganda, Rwanda na Burundi waendelee na Jumuiya hiyo. No problem!

Naona hata Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki nae kachoshwa. Ujanja ujanja wa kitoto kutoka kwa wenzetu umemchosha. Amesema jumuiya hiyo ni ya kusadikika. Kuwa baadhi ya nchi wanachama zinaendekeza unafiki na ubinafsi katika Jumuiya hiyo.

Alisema kuwa tatizo la ujanja ujanja na ubinafsi linaloonekana kuweka mizizi katika jumuiya hiyo, litaipeleka pabaya ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa kukomesha. Alisema Tanzania imejitolea kutoa elimu ya bure kwa nchi za EAC namna ya kupiga vita ukabila.

“Ukiniuliza tumefaidika nini nitakujibu badala ya mategemeo ya kupungua na kuondoa kabisa vikwazo vya kibiashara, ndiyo kwanza vimeongezeka.” Alisema.

Tatizo ni kuwa wenzetu wamekuwa wakijifanya wao ndiyo wajuaji sana wa Afrika. Hawana ardhi ya kutosha sasa wanataka kuhamia Tanzania. Eti ndiyo ushirikiano. Masihara hayo!

Jamaa wako kibao visiwani. Eti wanajua huduma kwa watalii. Utumbo mwingine! Sababu ni kuwa wanajua kiingereza. Hilo ni tatizo la muda tu. Ni sisi tuwafunze watoto wetu hicho kiingereza, kifaransa na hata kichina. Huwezi kufanya uamuzi wa kudumu kwa ajili ya tatizo la muda.

Hujifanya wanapendana na kupiga picha lukuki kwa ajili ya magazeti yetu, Watanzania wawaeleze wenzetu kuwa mtazamo na kasumba ya kujifanya wao ndiyo magwiji wa Afrika Mashariki hatuutaki.

Tuheshimiane na kuacha kabisa madharau hayo. Kama wataendelea na jumuiya yao, safi kabisa. Ila mambo ya kutaka kutuibia Watanzania ardhi yetu wasahau kabisa!

No comments: