Saturday, November 21, 2009

Wacha tu waendelee kuzipiga

Wiki mbili hizi kumekuwa na bonge la burudani kisiasa nchini kwetu. Mimi binafsi nimekuwa ni mmoja wa wananchi wanaoona kuwa mgogoro unaoendelea kwa upande fulani unamaslahi kwa WaTanzania. Nimekuzwa katika utamaduni wa kama mtu anataka kukuuzia ubabe wa kijinga na usiokuwa wa maana, basi kwanza mnatoka nje, mnananesa kwa ngumi na mateke, na atakayetoka na nundu shauri lake.

Nakumbuka, marehemu rafiki yangu mpenzi alikuwa akiwakatisha tama maadui zetu waliokuja na ngumi mkononi kwa kuwaambia kuwa ‘kupigana ni njia ya washenzi ya kupatana’

Wengine wamesema kuwa mgogoro unaotokea hivi sasa katika chama tawala ni wa kitoto. Mimi ninauangalia kimtizamo mwingine. Hao tunaowaita wazee nao pia walikuwa vijana siku moja. Wengine walikuwa hivyo hivyo, waadilifu, watu wa kuheshimika na watu poa kwa ujumla.

Wengine walikuwa chakaramu, wahuni, majitu ya hovyo kwa ujumla. Ila tu umri umewafanya walainike na kuficha makucha yao ya uzeeni. Lakini ukiwakwarua kidogo tu, wazee hao, wanarudia uchakaramu ule ule, na ukimuingilia hovyo atakupiga mabichwa usiyotegemea.

Sema tu wanatumia muda usiokubalika. Ukimuiona kijana asiyeenda disco akiwa na umri wa miaka 20 na, na kukimbizana na wenzie wa rika lake basi ujue kuna tatizo hapo. Na ukiona mzee wa miaka 55 anakwenda disco na kuanza kufukuzana na vijukuu vyake – eti wapenzi wake, napo hapo kuna matatizo makubwa.

Sasa tangu kupata uhuru, tumekuwa na chama kimoja cha siasa, ambacho kimefinyangwa kwa kiasi kikubwa na Baba wa Taifa, Hayati, Mwalimu Julius Nyerere. Ni yeye aliyekipa chama hicho heshima kubwa, kwanza kabisa kwa kujiheshimu yeye mwenyewe na kuwaheshimu wananchi wa Tanzania.

Wakati wa uhai wake, alisema tena na tena, umuhimu wa chama kuwa cha wakulima na wafanya kazi wa Tanzania. Aliwatilia ngumu sana majambazi yaliyotumia fedha kukinunua chama hicho. Lakini baada ya ya kumgoja Mwalimu apite njia yake hapa Ulimwenguni, majambazi hayo ya kisiasa, yameamua kuiteka nyara nchi nzima. Ndiyo wote huu ugomvi wao na vikaragosi vyao unaoendelea dhidi ya Watanzania.

Wengine wanasema kuna uwezekano wa chama tawala kugawanyika. Mimi sioni ubaya wowote kwa hilo. Ila ningependa wabunge mashujaa wenye kuipenda nchi yao wasiachie ngazi, hata wakidhalilishwa namna gani na wababe wa ‘Misheni Kota’ (Mission Quarters) Ilala, kama Sophia Simba na kundi lake. Wacha wababe, wao ndiyo waondoke na kuanzisha chama chao cha mafisadi.

CCM si chama kibaya. Ila kuna uchafu ambao unamahela, ambao wanataka kuendelea kufanya na kuendelea kufanya uovu wao kudhalilisha Tanzania. Majambazi hayo wacha yaendelee kuihujumu nchi yetu na tuone yatafika wapi. Hawawezi kundi la majambazi likaendelea kudhalilisha utu wa Watanzania kwa vipande 50 vya fedha.

Hali hii ya kuiendesha chi yetu kama gari bovu, haitaruhusiwa kuendelea milele. Hata Mwenyezi Mungu hatakubali uonevu huu. Mapambano yaendelee tu. Watanzania wanawajua mashujaa wao!

No comments: