Saturday, January 9, 2010

Jihadhari na mamluki wa uandishi!

Nimeliona jambo hili linatokea mara kwa mara kukiwa na uchaguzi au kama kuna tukio ambalo limelitingisha taifa kama vile kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na mawaaziri wawili. Naliona mwaka huu, linajirudia pole pole.

Jambo lenyewe ni kutokea kwa tabaka fulani katika fani yetu ya uandishi ya watu ambao huwezi kuwaita waandishi, bali mamluki wa fani hii.

Wakati wa uchaguzi uliopita wanasiasa waliajiri wazi wazi mamluki hao. Wao hawana maadili yo yote katika maisha yao. Wao wanachoabudu kiko katika madhabau (altar) ya fedha.

Watu kama hao watakupamba mpaka utaona kizinguzungu. Hawana aibu. Kama wewe ni jambazi lenye kuvaa suti, mamluki hao watasema wewe ni mkombozi na uishi milele, Amina!

Nakuwa wa kwanza kukubali kuwa wapo sana mamluki hao. Sasa hivi umetokea ujanja wa mamluki hao kutaka kuwakosha watu fulani waliotuibia mabilioni kuwa,eti, ni watu safi.

Kwanza mimi binafsi nashangaa kwa nini watuhumiwa hao wasichukuliwe hatua za kisheria? Nasema kila siku nchini hii mtu ukiiba kuku mmoja basi tunakuchoma na moto. Lakini ukiiba mabilioni – hapo sawa!

Mimi wala sitaupamba uhalifu huo mchafu na kuuita ufisadi. Nauita vile nilivyozoea – wizi! Mijizi imetuibia mabilioni, halafu sasa imeanza kupakaziana.

Tatizo la mwizi ni kusahau kuwa siku zake ni arubaini. Na jinsi ya kumpata mwizi ni kama ukitaka kumvua yule samaki wa baharini. Chuchunge.

Akiuma chambo wewe muongezee mshipi aende nao. Atakwenda weee-e-e! Akijua mambo shwari atameza chambo. Ndipo hapo utampata kwa ulaini.

We msomaji, unafikiria mambo hayo ya wizi baina ya viongozi tumeanza kutasikia leo? Wala! Tumeyasikia siku nyingi tu zilizopita. Lakini ukisema tu watu kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru wanakujia kama kifaru. Ushaidi uko wapi?

Mamluki wengine wanatafuta mambo ya ajabu kabisa. Ukabila.Eti akiwekwa mmasai mmoja hatiani basi kabila lake lote linaharibiwa jina na wengine kudhalilishwa. Utumbo mwingine huo. Hakuna kitu kibaya kama wapambe.


Wengine wanajidai kuwa wakati wa kuanza kampeni za uchaguzi nchini Tanzania hazijaanza. Wala msomaji asiamini madude hayo. Siku hizi kampani zinaanzishwa kila siku. Chini chini.

Unachotakiwa kufanya msomaji ni kuweza kusoma staili na mbinu tofauti wanazozitumia wanasiasa kufanikisha lengo hilo. Kwa sasa hivi mlengwa mkubwa ni yule mtu anayejiita mwandishi wa habari. Sisi wenyewe tunawajua. Wajomba hao wana njaa kali na wanasiasa wanawanunua wazi wazi.

Kimya kimywa tu unamuona bwana mdogo mmoja au kadada ghafla kanaanza kushabikia upuuzi wa fulani na kuuita habari. Nimeona Mbunge mmoja, yeye ni profesa, ghafla anashabikia mradi wa maji wa mjini Ilula, huko Iringa. Habari hiyo imetokea kwenye vijarida mtaani, kama mara tano hivi. Habari ile ile.

Mwanasiasa huyo ameisha mtia bwana maji wa Ilula jamba jamba, na kuuliza kwa nini maji hayatoki mjini Ilula. Jamaa amempa bwana maji siku 20 kueleza kwa nini Ilula iko kavu.

Swali ni kuwa, kwa nini sasa, kwa mbunge huyo kujifanya yeye ni bingwa wa kuleta maji mjini hapo. Mimi naona kama huo ni utani na kejeli kwa wananchi wa Ilula. Haya maji yanayoshinikizwa yatoke wakati huu yanatoka wapi? Ina maana kuanzia 2005 watu walikuwa hawajui maji mpaka alivyokuja mkuu na uchaguzi unaonekana huu umefika? Basi iko kazi.

Huku anakurupuka Waziri wa Utalii na Mali Asili, Shamsa Mwangunga amepiga marufuku safari za maofisa wake kusafiri kwenda nje kuzurura – wao wanaziita safari za kikazi. Eti kuendeleza utalii.

Kila mtu mwenye akili mzuri anajua kuwa sekta hiyo ya wizara ni ya wa wazururaji na watu wenye kwenda shopping kila siku. Sasa waziri huyo, baada ya kukaa kimya miaka, anasema amepiga marufuku safari hizo ambazo kwa msingi ni kudokoa fedha za walipa kodi. Hiyo ni danganya toto ya kila siku.

Mabilioni yemekuwa yanaliwa na maofisa wa serikali, na hata watu binafsi, kwa kusafiri nchi za nje. Huu mradi sasa umekuwa mkubwa kiasi ya kutia aibu. Lakini wao hawaoni hiyo. Sasa uchaguzi unakuja kila mjomba na anti wanajifanya nchi hii inawauma.

Shamsa hajatuambia lilicholotokea hasa hiko Loliondo, ambako waTanzania wa naonewa na kunyanyaswa na serikali yao. Shamsa hajasema wakoloni wa kiarabu wanaendeleaje na utawala wao wa sehemu kubwa kaskazini nchini Tanzania.

Nionavyo ni kuwa bado wabunge wengi hawana jipya la kusema na kwa watanzania wakati tukieleekea kwenye uchanguzi ujao mwezi Octoba. Wengi wa wapumbe wanasema hewa tupu. Wengi zaidi wanatayarisha shahada za PhD, juu ya kuwa kuwa wengi tumekubaliana kuwa hizo shahada ni hewa.

Lakini katika pumba nyingi unakuta watunga sheria wengine wanasema kunachowezekana kusikika. Napenda Mbunge Christopher ole Sendeka alivyowanyooshea wazazi wa Kiteto kidole kuwa yeyote atakaemzuia mtoto wa wa kike au yule ye yote yule,wa jimbo hilo la uchaguzi kutokwenda shule, astashitakiwa.

Sawa kabisa. Sheria hiyo ilikuwepo zamani na nilitegemea wabunge wangeivalia njuga sheria hiyo. Lakini naona wabunge wengu wako kwenye, kujenga U-dokta, na imaonyesha serikali nayo inanaafiki kuwepo kwa mafeki kibao kila mahala. Na huu ni mwanzo tu wa kasheshe itakavyokuwa mwaka huu.

Kuna hongo za kila siku katikakachuzi za nchini hapa. Sijui mwaka huu kutakua na nini kipya. Wasi wasi wangu ni kuwa sisi waTanzania tunaweza kufikitria kuwa hii nchi ni yetu, lakini mimi nina wasi wasi kuwa wajanja wanaweza wakawa wameiuza nchi hii zamani!

No comments: