Wednesday, August 12, 2009

Hakuna kama elimu. Lakini…

Nilikuwa kwenye kona yangu moja kijijini nikiangalia watu. Mimi napenda kuangalia na kusikiliza watu.

Kidogo nikaanza kumsikiliza aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam (Sasa ni kuu wa mkoa wa Mwanza), Abas Kandoro akianza ku-rap kuhusu mradi wa kujenga mashule mengi tu kwa ajili ya watoto wetu wa mkoa huu. Poa kabisa.

Baadaye nikamuona kwenye TV. Sitazungumzia kuhusu rangi mbaya za nguo alizovaa. Nazungumzia mambo aliyokuwa anayasema. Alisema maradhi, umaskini, elimu kuwa ndiyo adui tuliokuwa tunapambana kuanzia tumepata uhuru.

Akasema lakini adui mbaya zaidi ni kukosa elimu. Poa sana plus plus!
Hamna kitu kibaya kama jitu mbunju. Baya zaidi limbunju ambalo linajifanya janja. Yako kila mahali, serijkalini makanisani, miskitini na mengi zaidi mtaani.

Hivyo bwana 'legino' wetu wa Dar es Salaam akasema kuwa wanaDar es Salaam tuchagie kwenye mpango huo wa shule ili sekondari hizo zijengwe. Namuombea Braza Kandoro kila la kheri.

Namuombea kwa sababu mimi binafsi sitoi senti tano kwa mchango huo. Naona wametoa namba ya akaunti ya kuchanngia. Sichangi kwa sababu baado nina maswali lukuki ya kuuliza.

Nani atakuwa na mamlaka na uwezo wa kuzitoa fedha hizo. Mtu mmoja au kamati? Majina yao nani? Sitaki kuchangia mitaji ya wahuni.

Uoga wangu ni kuwa hizo fedha zikianza kurundikana katika akaunti hiyo kila mwana kamati ataanza kuweka ‘kampuni’ ya ndugu zake ili kuanza kizitafuna. Yametokea hayo hapa Bongo, wala si mageni.

Kwanza bwana michoro. Atakuwa ni shemeji wa mjumbe wa kamati hiyo? Halafu ujenzi utakua ni wa matofali. Nani ataleta matofari hayo? Fulani, ambaye ni hawara wa mwenyekiti wa kamati. Yametokea hayo!

Jee, nani atawaajili wachimba msingi? Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi ambaye atampa kazi hiyo kaka wa mchumba wake – yaani shemejie.

Nani ataleta simenti? Baba mdogo wa Katibu fulani katika serikali ya mkoa. Madawati je? Mchumba wa mwana kamati fulani. Haya! Nani ataleta madawati. Hayo yatakuja tu (Ingawa nasikia shule ya sekondari ya wasichana ya Msalato huko dodoma, wameanza kukaa sakafuni. Hakuna madawati)

Walimu je, watatoka wapi, Braza Kandoro? Zamani kazi ya waalimu ilikuwa inaheshimika sana. Siku hizi mtoto wako akisema anataka kuwa mwalimu kila mtu anamuona chizi!

Mimi ninashuku kuwa hizo fedha zitatafunwa na hakuna mtu ataulizwa swali lo lote. Fedha na mradi wa mabasi ya shule ya watoto wetu ziko wapi? Haya mchango wa madawati ya watoto wetu Dar es Salaam, nchango wake, ambao ulikuwa chini ya ofisi ya rais – fedha ziko wapi? Madawati yako wapi?

Ninachojua mimi kwa elimu dunia yangu, mtu anayeita watu wengune wachangie, kuna wengine wanangoja kuutafuna mchango huo. Kwa haraka sana nasema kuwa mkuu wetu wa mkoa anaweza kuwa na nia safi kabisa!

Lakini kuna wengine wanaongojea fedha ya kustaafu. Ukiwapa mwanya huo watazoa fedha hizo na kuingia mitini. Kwa kifupi ninawashuku wote wanaohusika na dili hii. Ni nani hao? Nani atasaini kutoa fedha hizo? Tutapata mahesabu kwa nani?

Sisi waBongo tumeumizwa sana na majambazi yanayovaa suti yakituambia utumbo kuhusu ‘maendeleo’ ya nchi yetu. Hasa wana maana maendeleo yao binafsi na familia zao!

Braza Abasi Kandoro ajue kabisa kuwa hilo si swala tu la kuchangia. Tunataka kujua nani watadhibiti fedha za wananchi. Tusije tukashikana makoo baadaye!

No comments: