Wednesday, August 12, 2009

Jihadhari na mamluki wa uandishi!

Nimeliona jambo hili linatokea mara kwa mara kukiwa na uchaguzi au kama kuna tukio ambalo limelitingisha taifa kama vile kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na mawaaziri wawili.

Jambo lenyewe ni kutokea kwa tabaka fulani katika fani yetu ya uandishi ya watu ambao huwezi kuwaita waandishi, bali mamluki wa fani hii.

Wakati wa uchaguzi uliopita wanasiasa waliajiri wazi wazi mamluki hao. Wao hawana maadili yo yote katika maisha yao. Wao wanachoabudu kiko katika madhabau (altar) ya fedha.

Watu kama hao watakupamba mpaka utaona kizinguzungu. Hawana aibu. Kama wewe ni jambazi lenye kuvaa suti, mamluki hao watasema wewe ni mkombozi na uishi milele, Amina!

Nakuwa wa kwanza kukubali kuwa wapo sana mamluki hao. Sasa hivi umetokea ujanja wa mamluki hao kutaka kuwakosha watu fulani waliotuibia mabilioni kuwa,eti, ni watu safi. Na wanaonewa tu na Kamati ya Wabunge wakiwa na mwenyekiti wao, Dr Harrison Mwakyembe. Kiyu ambacho ni utumbo mtupu.

Kwanza mimi binafsi nashangaa kwa nini watuhumiwa hao wasichukuliwe hatua za kisheria? Nasema kila siku nchini hii mtu ukiiba kuku mmoja basi tunakuchoma na moto. Lakini ukiiba mabilioni – hapo sawa!

Mimi wala sitaupamba uhalifu huo mchafu na kuuita ufisadi. Nauita vile nilivyozoea – wizi! Mijizi imetuibia mabilioni, halafu sasa imeanza kupakaziana.

Tatizo la mwizi ni kusahau kuwa siku zake ni arubaini. Na jinsi ya kumpata mwizi ni kama ukitaka kumvua yule samaki wa baharini. Chuchunge.

Akiuma chambo wewe muongezee mshipi aende nao. Atakwenda weee-e-e! Akijua mambo shwari atameza chambo. Ndipo hapo utampata kwa ulaini.

We msomaji, unafikiria mambo hayo ya wizi baina ya viongozi tumeanza kutasikia leo? Wala! Tumeyasikia siku nyingi tu zilizopita. Lakini ukisema tu watu kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru wanakujia kama kifaru. Ushaidi uko wapi?

Mamluki wengine wanatafuta mambo ya ajabu kabisa. Ukabila.Eti akiwekwa mmasai mmoja hatiani basi kabila lake lote linaharibiwa jina na wengine kudhalilishwa. Utumbo mwingine huo. Hakuna kitu kibaya kama wapambe.

Tunaambiwa Lowassa alipokelewa kifalme Monduli. Na kwamba kiasi cha watu elfu kumi wa jimbo lake walijitokeza kumlaki na idadi ya magari ilikuwa ni 400! Poa kabisa! Na zulia jekundu lilitandikwa. Wameandika mamluki hao.

Mimi hayo ya magari elfu au watu 10,000 au 50,000 hayanihusu. Ninachotaka kujua ni hela yetu iliyoibwa kwa kutumia makampuni feki iko wapi? Na hayo magazeti yanayowapigia ndogo ndogo yale majizi ni ya nani hasa? Si ya swahiba wao Rostam Aziz? Sasa?

1 comment:

Alecia 101 said...

i think its a simple solution. The fewer temptations, the better. We should do away with such funds, they only lead to foreseeable trouble.